Usajili wa laini za simu kufanyika kielektroniki
Serikali ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kupitia mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeyaamuru makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi Tanzania, kusajili wateja wake kidigitali kwa kutumia programu maalumu inayofanyakazi kwenye simu Janja (smartphone) ambayo inajulikana kama KYC/eKYC (Know your Customer).
Agizo hilo limekuja kutokana na udanganyifu unaofanyika katika usajili ambapo watu walikuwa wanatoa taarifa za uongo wakati wa usajili, ikiwa ni pamoja na kusajili bila vitambulisho ama kutumia vitambulisho vya watu wengine, kitu ambacho ni kinyume na sheria.
Udanganyifu huo ulikuwa unaipa taabu serikali pindi mteja aliyesajiliwa kidanganyifu anapofanya uhalifu kwa kutumia laini yake, kama vile kuiba fedha, kutukana watu kupitia simu, kufanya mauaji, n.k. Kukamatwa kwa wahalifu wa aina hiyo ilikuwa inaleta ugumu kutokana na taarifa za usajili kutokuendana na taarifa sahihi za wahalifu.
katika aina hii ya usajili wa kielektroniki, mteja anatakiwa awe na kitambulisho halali kinachokubalika kutumika kwenye usajili wa laini za simu za mkononi. Mamlaka ya mawasiliano imeruhusu aina tano (5) tu ya vitambulisho ambavyo vitakuwa vikitumika katika usajili, ambavyo ni Kitambulisho cha Taifa, Kadi ya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Pasi ya Kusafiria pamoja na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.
Pia mteja hapaswi kutoa nakala ya kitambulisho chake anapokwenda kusajiliwa, na badala yake, anatakiwa aende ana kitambulisho chake halisi na wakala atakipiga picha wakati wa usajili kwa kutumia mfumo wa kusajili.
Hali kadhalika mteja anatakiwa kupigwa picha ya sura yake (usoni) kwa ukubwa wa passport size, ambapo sambamba na picha ya kitambulisho picha ya sura ya mteja huambatanishwa na hutumwa moja kwa moja kwenye Database ya TCRA na ya kampuni husika (k.v Tigo, Zanztel, Airtel, Smart. n.k). Taarifa hizo zikishafika katika database hukaguliwa na maafisa walioajiliwa kwa ajili ya ukaguzi ili kubaini kama usajili ni wa halali au batili.
Ikigundulika kuwa usajili ni batili laini inafungwa inasitishiwa huduma zote, kwa hiyo mteja hawezi kupiga wala kupigiwa simu pamoja na huduma nyingine. Hii ni kwa ajili ya kudhibiti mteja mwenye usajili batili asitumie laini kwenye matukio ya kihalifu kama vile kutapeli, kukashifu watu au kufanya tukio lolote ambalo ni kinyume cha sheria.
Mambo yanayoweza kupelekea usajili kubatilishwa au kukataliwa ni pamoja na wakala/freelancer kuingiza taarifa za mteja ambazo zinatofautiana na zile zilizomo kwenye kitambulisho cha mteja. Taarifa hizo zaweza kuwa majina, tarehe ya kuzaliwa, n.k. Wakala anaweza kukosea kuingiza taarifa kwa bahati mbaya au anaweza kuingiza taarifa za uongo kwa makusudi kwa tamaa ya pesa hususan kama mteja ana kitambulisho cha mteja mwingine.
Kingine, ni kupiga picha sura ya mtu mwingine badala ya mmiliki halisi wa kitambulisho, au kupiga picha nakala ya kitambulisho badala ya kitambulisho halisi. Pia wakala akipiga picha isiyoonekana vizuri (blur) usajili wa laini husika utakataliwa sambamba na kusitishiwa huduma zote.
Mfumo huo wa eKYC una uwezo wa kutambua sura ya mtu kwa hiyo wakala/Freelancer akiielekeza kamera katika sehemu isiyo na sura ya mtu mfumo hautachukua picha hadi pale kamera ikielekezwa pahala penye sura ya mtu na anapaswa awe katika umbali wa mkono moja. Wakala hapaswi kubofya kitufe cha kuruhusu kamera kupiga picha, bali picha itachukuliwa automatikali baada ya mfumo kukamata sura ya mtu.
Pia Simu inayotumika kwenye usajili inatakiwa iwashwe data, GPS na iwe na kifurushi cha Intaneti kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji wa taarifa kutoka kwa wakala kwenda kwenye database.
Mfumo huu wa kusajili kwa kutumia Smartphone una faida nyingi kwa upande wa mawakala, serikali pamoja na kampuni zinazotoa huduma za simu za mkononi. faida kubwa ni pamoja na kudhibiti wizi wa kimtandao, kuondoa udanganyifu katika usajili, kumuondolea wakala majukumu ya kujaza fomu za usajili na kuondoa usumbufu kwa wakala au kwa wateja wa kwenda steshenari kutoka nakala za vitambulisho vya wateja.
Related Articles
Habari za michezo
Timu zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi Zanzibar 2017
Yanga yaichapa 2-0 Zimamoto FC
Simba SC yazidi kusonga mbele kwenye michuano ya Mapinduzi Cup
Simba SC yailambisha mabao 2-1 timu ya Taifa Jang'ombe
Yanga yaichapa Jamhuri mabao 6-0 katika michuano ya Mapinduzi Cup
No comments:
Post a Comment