Hotuba ya Dkt. Hamisi Kigwangalla, alipopokelewa Jimboni Nzega Baada ya Kutangaza nia Kugombea Urais wa Tanzania
NzegaAwali ya yote nianze kwa kumshukuru mwenyezi mungu, mwingi wa rehema na mwenye kurehemu, kwa kutujalia afya njema na kutukutanisha hapa siku hii adhimu ya leo, maana ni kwa utashi wake tu tunaweza kuyafanya haya yote.
Nitumie fursa hii kwa namna ya kipekee kuwashukuru nyote kwa kuacha shughuli zenu kuja kunipokea na kushiriki mkutano huu. Mmenipa heshima kubwa sana na mimi nawajibika tu kusema ‘ahsanteni sana.
Mimi hapa ni aidha mtoto wenu, mjukuu wenu ama mdogo wenu, mnapoacha shughuli zenu kuja kunisikiliza mimi, mnakuwa mmenitwisha mzigo mzito sana. Ninajiona nawajibika kwenu kutoa utumishi uliotukuka. Ninajipa deni la kuongeza bidii kubuni miradi itakayotatua shida zetu hapa Nzega, kupigana kuondoa umaskini, ujinga na maradhi.
Sote tuliopo hapa ni mashahidi, kuwa tumefanya mengi katika miaka hii minne ya uwakilishi wangu, maana kati ya hayo, mengi tumefanya pamoja nanyi.
Tumeanzisha ujenzi wa High Schools nne, na zote ziko katika hatua nzuri za utekelezaji. Tumeanzisha ujenzi wa barabara mpya zaidi ya 10 huko vijijini, barabara za lami zaidi ya km 10 hapa mjini, tumejenga zahanati zaidi ya 20, tumejenga nyumba za walimu na wahudumu wa afya zaidi ya 30 huko vijijini, tumechimba visima zaidi ya 40 huko vijijini, tumefanikisha kufufua kilimo cha zao la pamba na kukuza uzalishaji toka Kg 20,000 mwaka wa kwanza mpaka zaidi ya Kg milioni 8 mwaka wa tano wa mradi, tumeweza kukuza uzalishaji wa zao la alizeti toka Kg 50,000 mwaka wa kwanza wa mradi mpaka zaidi ya Kg milioni 2 mwaka wa tatu wa mradi, tumeweza kuanzisha SACCOS mpya 9 na vikundi vya kushirikiana kiuchumi zaidi ya 100, tumeweza kuanzisha mradi wa kuandikisha wanachama wa SACCOS, vikundi vya ushirika na vikundi vya kibiashara kwenye hifadhi ya jamii ya NSSF. Tumeweza kulipia ada zaidi ya watoto 600 wanaotokea familia zenye uwezo duni kiuchumi na yatima.
Tumeweza kudai haki yetu ya ushuru wa huduma na miradi ya maendeleo toka Resolute Tanzania Ltd na kufanikiwa kupata zaidi ya bilioni 3 na nusu mpaka sasa, na kujengewa High School kule Lusu, Kituo cha afya kule Lusu, mabwawa ya maji vijijini, kurekebishiwa mitambo ya kusafisha maji yanayokuja hapa mjini na kujengewa maabara 10 kwenye shule zetu za Sekondari. Tusingedai haya, kwa hakika tusingepewa. Orodha ni kubwa mno, siwezi kuyataja yote hapa.
Nitakuwa mtovu wa shukrani nisipokubali na kutambua ushiriki wa karibu wa nyie wananchi wenzangu wa Jimbo la Nzega, Mbunge mwenzangu wa Jimbo la Bukene, Madiwani wa Halmashauri yetu, Viongozi wenzangu kwenye Chama changu, Viongozi wa vyama rafiki, Mkuu wa Wilaya, na Mkurugenzi na timu yake yote.
Leo si siku ya kukumbuka mapito yangu lakini ni siku ya kutambua na kuthamini ugumu wa njia ya kuelekea mafanikio, ili tunapotamani kusonga mbele tujue kinachotusubiri. Ugumu wa safari yangu umenipa umahiri, ujuzi zaidi, ujasiri na uzoefu utakaohitajika sana kwenye ‘safari ya kuamini’ (a journey of believe) niliyotangaza kuianza.
Ugumu wa safari yangu umethibitisha usemi kuwa kwa hakika mti wenye matunda matamu ndiyo unatupiwa mawe; falsafa hii ilinipa nguvu ya kujitazama upya, kujitathmini na hatimaye kufanya uamuzi sahihi kuhusu hatma yangu kisiasa na Tanzania yangu.
Si ugumu wa safari yangu kisiasa pekee ulionipa ujasiri na utambuzi wa wajihi na uwezo wangu kiuongozi, bali pia historia ya makuzi yangu, na mahitaji, matarajio, matamanio na kero za watanzania wenzangu.
ROHO YA UTHUBUTU
Nilipokuja nyumbani kugombea Ubunge kwa mara ya kwanza, mwaka 2005, nilikuwa ndiyo kwanza tu nimehitimu mafunzo yangu ya digrii ya udaktari, na nilikuwa kwenye mafunzo ya kazi ya udaktari kwa vitendo chini ya usimamizi wa madaktari bingwa (yaani internship), sikuwa na ajira ya kudumu. Sikuwa na uchumi wa kutisha. Nilikuwa nina ndoa changa sana. Sikuwa na nyumba nzuri wala gari ya kifahari. Niliamini kwa kuwa mimi ni mzaliwa wa hapa, nina ndugu na marafiki wengi, itawezekana tu kuwashawishi na kushinda ubunge. Sikujua kuwa kuna zaidi ya undugu na urafiki kwenye siasa. Hii inaitwa ‘Roho ya Uthubutu.
ROHO YA KUTOKATA TAMAA
Kuna baadhi ya watu mwaka ule walinikejeli na kucheka sana, kuna ndugu zangu na marafiki mbalimbali wa familia yetu walinikwepa kwa kuwa tayari waliishatekwa na kambi nyingine. Hekima yangu ndogo ya ujana ule ilinituma kuheshimu uamuzi na uchaguzi wao, maana ndiyo demokrasia, na nilichokifanya ni kuendelea kuwaomba kura na kuwachangamkia kana kwamba tupo nao pamoja.
Japokuwa niliona nafasi ya kushinda kwangu ni ndogo sana, sikukata tamaa, nilijipa moyo na kuendelea kutumia fedha ndogo nilizokuwa nazo kuwafikia wananchi wa jimbo letu katika kila kona. Hii inaitwa ‘Roho ya Kutokata Tamaa.
LIFT HUMKUTA ALIYE NJIANI!
Mwaka 2010 nikatia nia tena kuja kugombea Ubunge wa jimbo la Nzega, mara hii nikiwa mgombea bora zaidi, mwenye matayarisho ya kutosha. Kilichonitokea, sote hapa mashuhuda.Watu walioamini tumechezewa mchezo mchafu walikuja nyumbani kwangu baada ya matokeo ya kura ya maoni, wengine na mabarua ya kukata rufaa na ushahidi wa kilichofanyika, wengine na mapicha, wengine wakilia, wengine wakitoa matamko makali sana dhidi ya viongozi wenzangu chamani, wengine wakinishawishi nihame chama. Niliwatuliza, nikanyamaza, nikaondoka Nzega. Mungu si Athumani, chama changu kikanipa fursa ya kukiwakilisha kwenye uchaguzi ule. Nami sikukiangusha. HII INAITWA: ‘Lift humkuta aliye njiani.
NCHI TAJIRI YENYE WATU MASKINI
Tanzania ni nchi tajiri sana lakini wananchi wake ni maskini sana. Tanzania ina urithi wa kutosha wa watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Ni nchi yenye mlima mrefu kuliko yote Africa, ziwa lenye kina kirefu kuliko yote Afrika, madini ya dhahabu na vito, gesi, ardhi yenye rutuba na mabonde mengi ya nafaka, ng’ombe wengi, mito, maziwa, na watu wenye nguvu, wastaarabu wanaopendana, walioshikamana kwa umoja wao na wanaoheshimiana na kuvumiliana kwa tofauti zao.
Hizi ni tunu tulizorithi kwa wazee wetu. Waasisi wa Taifa hili waliweka misingi ya nchi hii kufanikiwa. Waliweka misingi ya Tanzania kutajirika. Hili ni fumbo kwa kizazi chetu.
Waasisi waliweka misingi ya kuthamini utu wa kila mmoja wetu, usawa wa kila binadamu, umoja na mshikamano wa kitaifa, uhuru na mfumo wa kutuondoa kwenye umaskini na kutupeleka kwenye uchumi imara wa kujitegemea.
Waasisi waliweka mfumo wa elimu ulionitoa mimi uswahili kwetu Msoma Road na kunipeleka kwenye ulimwengu wa wasomi kwenye makorido ya vyuo vikuu mashuhuri duniani. Waliweka mfumo ulionitoa mimi kwenye lindi la umaskini wa kula mlo mmoja na kwenda shuleni bila viatu mpaka ulimwengu wa kujenga hoja Bungeni na kuota ndoto ya kuwa Rais wa nchi yangu.
Wazazi wetu waliorithi nchi hii kwa waasisi wa taifa letu wamefanya makubwa. Wameandaa mazingira na mikakati ya kututoa kwenye uchumi wa nchi maskini zaidi duniani. Dira yetu ni kutoka huku na kuingia kwenye uchumi wa daraja la kati kufikia mwaka 2025. Hii ina maana kwamba Rais atakayerithi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete atapaswa kuwa wa kwanza kuiongoza Tanzania tajiri, Tanzania ya ndoto za waasisi wa Taifa letu.
JUKUMU LA KIZAZI CHETU
Waliotutangulia wamefanya kazi yao. Ni jukumu la kizazi chetu sasa kuchukua wajibu huu mzito wa kuliongoza Taifa hili kufikia ndoto za mababu zetu.
Ndoto za kwamba, tulipojitawala tulitaka uhuru wa kujitawala wenyewe, uhuru wa kujiongoza wenyewe, uhuru wa kuchagua tunachotaka kufanya, uhuru wa kuamua kuwa tunavyotaka.
Jukumu letu sasa ni kuhakikisha kuwa wale mama ntilie na wamachinga wanaonyanyaswa kila siku na mgambo wa halmashauri zetu wanapewa uchaguzi murua wa kufanya biashara zao kwa uhuru na ustawi bila wasiwasi wa kumwagiwa chini chakula chao ama kunyang’anywa mali zao.
Wale wachimbaji wadogo wadogo wanaonyanyaswa na mfumo kwa sababu ya ujio wa kasi wa ubepari na soko huria na ule wimbo mwanana wa ‘dunia ni kijiji’ na mwaliko wa wawekezaji kwa kisingizio cha kuleta mitaji na teknolojia nao wana haki na uhuru wa kuchagua kuwa wachimbaji wa dhahabu, na ni lazima awepo mtu atakayehakikisha kuwa uchaguzi wao wa kazi hii unalindwa na mfumo wa uchumi wetu.
Wale waalimu, wauguzi, askari polisi, maafisa ugani na watumishi wenzao wa umma waliojitolea kukubali kufanya kazi kwenye maeneo ya mbali na mikoa ambayo ni ‘center’ kubwa za nchi na za wilaya zao, na wakakubali kuishi kwenye nyumba zisizo umeme wala maji ya uhakika, wakakubali kuishi kwenye vijiji visivyo na mawasiliano ya simu wala ya intaneti, wanastahili kutambuliwa na kuthaminiwa kwa kuwa wanafanya kazi iliyowashinda wenzao. Lazima awepo mtu atakayewawekea mfumo wa kipekee wa motisha unaoendana na uwiano wa umbali, jiografia na mazingira ya kazi.
Kwa akili ya kawaida tu, hatupaswi kuwalipa sawa walimu wetu wa shule ya Sekondari Chifu Ntinginya na wale wa Shule ya Sekondari Mwakashanhala. Mwakashanhala walimu wako wanne, na nyumba iko moja. Wote wanaishi humo. Wa Mwakashanhala hana mahali atapata nyumba ya kupanga. Wa Nzega Mjini ana chaguzi za kutosha za nyumba za kupanga.
Wale wakulima wanaotengeneza zaidi ya asilimia 80 ya nguvu kazi ya Taifa letu ni lazima wapewe huduma bora za ugani, walime kisasa na kwa tija; wajengewe miundo mbinu ya umwagiliaji, ili walime na wavune kwa uhakika.
Wale wazee, walemavu, akina mama wajawazito na watoto wapate ile haki yao ya kutibiwa bure mahospitalini bila kutakiwa kwenda kununua dawa ama vifaa kwenye vituo vya private. Ni kwa faida gani sasa tunasema tunawapa huduma za afya bure wakati hatuna dawa za kuwapa, ama vifaa vya kutolea huduma?
Ni jukumu la viongozi wa kizazi hiki kubuni mbinu mpya za kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora na za uhakika kwa kila mtanzania; kwamba, watanzania wote wanakuwa na bima ya afya na bima ya maisha; kwamba watanzania wote wanakuwa na hifadhi ya jamii bila kujali wapo kwenye ajira rasmi ama ni wakulima, wajasiriamali ama wachuuzi wadogo wadogo.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi hiki kubuni mbinu mpya za kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na motisha ya kufanya ugunduzi na ubunifu; kwamba, watoto wetu wanapenda zaidi masomo ya sayansi na wanakuza vipaji vyao.
Kwamba, wanamichezo wetu na wasanii wanang’aa si tu ndani ya mipaka ya nchi yetu bali pia kimataifa na wanafaidika na kazi ya ubunifu wao. Ni jukumu la viongozi wa kizazi chetu kubuni mbinu mpya zitakazodumisha nidhamu ya kazi na uwajibikaji, uzalendo na uadilifu, na zitakazotokomeza mbali kabisa rushwa, ubadhirifu, unyonyaji, ukandamizaji, wizi na matumizi mabaya ya ofisi za umma.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi chetu kuhakikisha tunatanua mtandao wa barabara zetu, tunaongeza ufanisi wa reli na bandari zetu, tunarahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa baina ya mikoa yetu, tunaongeza ufanisi katika mfumo wa biashara zetu za ndani na za kimataifa.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi chetu kuhakikisha tunaboresha mfumo wa kibenki toka vijijini mpaka mijini ili kuona wakulima na wafanyakazi wetu kule vijijini wana fursa za kupata huduma za kifedha na mikopo, na wale wafanyabiashara wakubwa wanapata fursa za kuuza bidhaa zinazozalishwa nchini kwa faida na kwa urahisi.
Tanzania ya leo si Tanzania ya mwaka 1990. Nzega ya leo si Nzega ya mwaka 1985. Wazee wa leo si wale wa miaka ile. Sura nyingi ni ngeni, si zile za utoto wangu. Nyumba nyingi ni mpya, si zile za uswahili kwetu Msoma road.
Barabara za Nzega ya leo si zile za miaka ya 2000. Kila kitu kimebadilika. Uongozi wa Taifa letu hauwezi kubaki ule ule. Majina ya viongozi wa Taifa letu hayawezi kubaki yale yale. Fikra za kuongoza Taifa haziwezi kubaki zile zile. Staili ya kuleta mapinduzi haiwezi kuwa ile ile.
WAZEE WETU WAMEWEKA MATUMAINI KWETU
Wazee mashuhuri wa Taifa hili wako wapi leo hii? Wazee mashuhuri wa Nzega wako wapi leo hii? Akina Mzee Mshindo, akina Mzee Ramadhani Mtwale, akina Sheikh Abdallah Kassa, akina RR Nyembo, akina Chief Kisute, akina Chief Humbi, akina Chifu Msoma, akina Chifu Ntinginya, akina Ibhambangulu, wako wapi leo hii? Wote hawa walitenda mambo ya hekima katika uhai wao, wakawa wenye kuvuma kwa sifa zao na matendo yao. Nasi tukajifunza kwao, tukapata ujasiri, tukapata umahiri, tukapata hekima, tukapata nguvu ya kutamani kufanya makubwa kwa ajili ya Nzega yetu, na makubwa zaidi kwa ajili ya Taifa letu.
Huko waliko wazee wetu najua wanatutazama na kutabasamu bila shaka wakiamini kuwa majukumu waliyotuachia tunayaweza. Nasi tunawaahidi kuwa tutawaenzi kwa kutenda yaliyo mema kwa Taifa letu na watu wake, kwa Nzega yetu na watu wake.
UONGOZI NA UJANA
Kuna watu wanakejeli ndoto za viongozi wenye taswira ya ujana kama mimi, wanadhani na wanaamini kuwa uongozi ni uzee na uzoefu. Mimi siwashangai wala sitaki kuwapinga, na hapa simaanishi kuwajibu. Ila nataka wafahamu ya kuwa uzee ama ujana siyo sifa pekee ya kuwa kiongozi mzuri.
Kuna vijana walipewa uongozi bila ya kuwa na uzoefu wowote ule kwenye serikali: akina Tony Blair wa Uingereza, Lee Kuan Yew wa Singapore, Thomas Sankara wa Burkina Faso,Mwl. Julius Nyerere, Baba wa Taifa letu, hawa wote walifanya makubwa ya kupigiwa mfano. Kuna wazee walipewa uongozi, na wakafanya mabaya na ya aibu kubwa si tu kwa mataifa yao, hata kwa walimu wao na familia zao.
Mimi ninaamini Tanzania ya leo inahitaji kiongozi mbunifu, mweledi, mwenye uthubutu, mwenye msimamo thabiti, mwenye uzoefu wa dunia ya biashara, dunia ya haki, fursa na usawa kwa watu wote, dunia ya utandawazi na diplomasia ya kiuchumi, dunia ya utawala bora, awe anamuogopa Mungu lakini asiyetumia dini kama silaha ya kimkakati ya kumpa uongozi, na mzalendo anayechukia rushwa, pia asiyetumwa na kundi lolote lenye maslahi; na sifa kubwa kuliko zote awe anayeweza kuleta mapinduzi ya mfumo wa uendeshaji nchi. Kwamba awe mzee ama kijana, kwangu si hoja sana.
Uongozi ni kuwa tayari kusikiliza kero na matatizo ya unaowaongoza, ukajua yanayowasibu na ukajipanga kuyatafutia ufumbuzi. Uongozi ni kujua mahitaji, matamanio na matarajio ya watu wako, ni kujua ndoto zao na ukazitafutia namna ya kuzitimiza. Uongozi ni wito wa utumishi kama ulivyo udaktari, ualimu ama utumishi wa Mungu.
Uongozi wetu katika zama hizi ni lazima uwe wa kimapinduzi na wenye fikra mpya na zinazoendana na wakati, unaoweza kuleta mabadiliko katika hali za watanzania kwa haraka na kwa uhakika. Ni lazima ujue kuwa hatuwezi kuendelea bila kuwa na mfumo imara wa kilimo na viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo, mfumo ambao utazalisha ajira za kutosha kwa watu wote, kuanzia wakulima wadogo mpaka wakubwa, wafanyabiashara, wasomi na wachukuzi.
HITIMISHO
Ndugu wananchi wenzangu wa Nzega, nimalize kwa kuwashukuruni nyote, kwa mara nyingine tena, kwa kuja kunipokea nyumbani, na zaidi kwa kunisikiliza. Nimalize kwa kusema kuwa; tulianza safari ya kuamini kwa kumuomba Mungu aliye juu, niwahakikishie kuwa tutaendelea kuwa naye safarini na tutamaliza naye, na kwa hakika Mungu atafanya maajabu yake; maana hajawahi kushindwa na kitu.
Mungu awabariki sana. Mungu ibariki Nzega, Mungu ibariki Tanzania.
Paul Makonda aanza ziara ya siku 10 ndani ya jiji la Dar Es Salaam
November 19, 2016
Rais Magufuli afanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi za mashirika ya hifadhi za jamii
November 19, 2016
Dr. Shein azindua wodi ya watoto na wazazi
November 19, 2016
Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA
November 20, 2016
No comments:
Post a Comment