Simba SC yailambisha mabao 2-1 timu ya Taifa Jang'ombe
Zanzibar, TanzaniaSimba Sports Club, almaarufu wazee wa msimbazi wameianza vizuri michuano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar 2017, baada ya kuicharanga mabao 2-1 klabu ya Taifa Jang'ombe. Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan usiku huu mjini Unguja, ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa timu ya Simba tangu kuanza kwa michuano ya kombe hilo tarehe 30/12/2016.
Simba wamefanikiwa kunyakua point 3 za ushindi katika mechi hiyo kutokana na magoli 2 yaliyozamishwa langoni mwa timu ya Taifa jang'ombe na wachezaji Mzamiru Yassin na Juma Luzio. Mzamiru alipachika bao la kwanza kunako dakika ya 28 katika kipindi cha kwanza, baada ya kumalizia mpira uliokuwa umerudi uwanjani baada ya kugonga nguzo ya goli.
Juma Luzio alizitikisa nyavu za lango la Timu ya Taifa Jang'ombe kunako dakika ya 42 katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, baada ya kuwatoka kwa kasi kubwa walinzi wa timu ya Taifa Jang'ombe na kuachia shuti kali iliyopita mlinda mlango wa Taifa jang'ombe akiwa hana namna ya kuuzuia mpira huo.
Simba SC walionekana kuutawala sana mchezo katika kipindi cha kwanza, ambapo wenyeji wao walionekana kuzidiwa nguvu katika kipindi chote cha kwanza, licha ya kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa timu ya Simba ambayo hayakuweza kuzaa matunda. Hadi kipenga cha mapumziko kikipulizwa wekundu wa msimbazi walikuwa wanaongoza mchezo kwa magoli 2-0 dhidi ya wenyeji wao, Taifa Jang'ombe.
Katika kipindi cha pili Taifa jang'ombe waliweza kubadilika na kufanya mashambulizi makubwa kuelekea katika lango la timu ya Simba SC, hususan baada ya kufanya mabadiliko katika safu ya ushambuliaji. Mashambulizi hayo yaliwapatia goli la kufutia machozi vijana hao wa Jang'ombe, baada ya mchezaji wa nyuma wa Simba SC Novaty Lufungo kujifunga alipokuwa anaokoa mpira uliokuwa umepigwa kutoka pembezoni mwa uwanjani.
Taifa Jang'ombe walichemka zaidi katika dakika za mwisho ambapo wekundu wa msimbazi walionekana kuzidiwa nguvu, hivyo kuwapa nafasi vijana wa Mitaa ya Jang'ombe kufanya mashambulizi ya nguvu katika lango la Timu ya Simba SC. Pamoja na mashambulizi hayo, Taifa Jang'ombe hawakufanikiwa kuongeza goli jingine, na hadi kipenga cha kufunga mchezo huo kikipulizwa, simba ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Aidha, Taifa Jang'ombe leo walikuwa wanacheza mechi ya pili katika michuano hii, ambapo katika mechi ya kwanza walicheza na mahasimu wao, Jang'ombe Boys ambapo waliibuka na ushindi wa goli moja (1) dhidi ya Jang'ombe Boys. Kwa upande wa Simba, leo ilikuwa mara yao ya kwanza tangu kuanza kwa mashindano haya.
Mechi nyingine iliyochezwa leo iliwakutanisha wakusanya mapato kutoka Uganda (URA) na KVZ ya Zanzibar, ambapo URA waliibuka na ushindi wa goli moja (1) na kujikusanyia pointi zote tatu za mchezo huo.
Related Articles
Yanga yaichapa Jamhuri mabao 6-0 katika michuano ya Mapinduzi Cup
Timu ya Yanga almaarufu wakimataifa, wameianza vizuri michuano ya Mapinduzi Cup 2017, inayofanyika kila mwaka mjini Zanzibar, baada ya kuwachapa mabao 6-0 walima karafuu wa Pemba, Jamhuri, katika mchezo uliopigwa usiku huu kwenye uwanja wa Amaan uliopo katikati ya mji wa Zanzibar...
No comments:
Post a Comment