Simba SC yamtoa nje Yanga Kombe la Mapinduzi
Zanzibar, TanzaniaWekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club, wamefanikiwa kuzizima ndoto za mtani wao wa Jadi, Dar Young Africans, za kuchukua Kombe la Mapinduzi Zanzibar 2017, baada ya kuitandika Yanga mikwaju ya matuta 4-2, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa leo saa 2:15 usiku.
Mchezo huo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, huku kila timu ikiwa na lengo la kupata ushindi ili ifuzu kwenda fainali. Yanga walikosa magoli kadhaa katika kipindi cha kwanza. Halikadhalika Simba SC pia walikosa magoli ya wazi husuan lile la dakika za mwishoni za kipindi cha kwanza ambapo mshambuliaji, Juma Luizio alipiga nje ya goli baada ya kupata mpira uliorudi kufuatia shuti kali iliyogonga nguzo ya lango la Yanga.
Hadi kipindi cha kwanza kinakwisha, hakuna timu iliyokuwa imeliona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili kilianza kuwafurahisha zaidi mashabiki wa Simba kutokana na wachezaji wa simba kucheza mchezo kwa kuelewana, huku wakikosa kosa mabao katika lango la Yanga, hali iliyowapa matumaini wana Msimbazi kuwa huenda magoli yalikuwa yananukia katika lango la timu ya Yanga.
Yanga waliweza kuumili mpira dakika za 70, ambapo walianza kusumbua sana, na kuanza kutishia kuzifumania nyavu za timu ya Simba. Hadi dakika 90 znakwisha, hakuna timu iliyokuwa imemfunga mwenzake, kwa hiyo ilibidi mchezo uelekee kwenye matuta ambapo, simba waliibuka washindi kwa kufanikiwa kufunga mikwaju 4 huku wakipoteza 1 tu, huku Yanga wakiambulia 2 na kukosa 3.
Waliofunga mikwaju katika timu ya Simba ni Nahodha Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Muzamiru Yassin na beki Janvier Bokungu, huku penati ya Beki Mzimbabwe, Method Mwanjali ikiokolewa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi almaarufu ‘Dida’.
Waliofunga penati kwa upande wa timu ya yanga ni Msuva na Thabani Kamusoko, huku mlinda wa mlango wa Simba SC, Daniel Agyei akiokoa mikwaju ya Dida na Mwinyi Hajji Mngwali.
Kwa matokeo hayo Simba SC imefuzu kwenda fainali ambapo itakutana na wanalambalamba, Azam ambao wamefanikiwa kwenda fainali baada ya kuitandika timu ya Taifa Jang'ombe bao 1-0 katika mchezo waliocheza jioni ya leo kwenye uwanja wa Amaan, mjini Ungauja, Zanzibar.
Aidha, Simba SC imeitonesha kidonda timu ya Yanga kwa kipigo hicho, kwani katika mechi yake ya kufunga mzunguko wa kwanza wa michuano hiyo iliadhibiwa mabao 4-0 kutoka kwa Azam. Pia ushindi huo wa Simba umewapa furaha zaidi mashabiki wake ambao walikuwa wanatiwa hofu na tambo za mashabiki wa Yanga waliokuwa wanajigamba kuwa yanga itaibuka na ushindi dhidi ya Simba SC na kwamba Kombe la Mapinduzi 2017 litapelekwa Jangwani.
Related Articles
Simba SC yailambisha mabao 2-1 timu ya Taifa Jang'ombe
Simba Sports Club, almaarufu wazee wa msimbazi wameianza vizuri michuano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar 2017, baada ya kuicharanga mabao 2-1 klabu ya Taifa Jang'ombe. Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan usiku huu mjini Unguja, ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa timu ya Simba tangu kuanza kwa michuano ya kombe hilo tarehe 30/12/2016...
Yanga yaichapa Jamhuri mabao 6-0 katika michuano ya Mapinduzi Cup
Timu ya Yanga almaarufu wakimataifa, wameianza vizuri michuano ya Mapinduzi Cup 2017, inayofanyika kila mwaka mjini Zanzibar, baada ya kuwachapa mabao 6-0 walima karafuu wa Pemba, Jamhuri, katika mchezo uliopigwa usiku huu kwenye uwanja wa Amaan uliopo katikati ya mji wa Zanzibar...
Habari nyingine
URA yashindwa kutamba mbele ya Simba SC, Mapinduzi Cup
Azam FC yalazimishwa sare na Jamhuri FC ya Pemba
Timu zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi Zanzibar 2017
Yanga yaichapa 2-0 Zimamoto FC
Simba SC yazidi kusonga mbele kwenye michuano ya Mapinduzi Cup
No comments:
Post a Comment