Baa la njaa lawatenganisha wanandoa, Sengerema
Sengerema, MwanzaWakati mvutano mkali ukiendelea baina ya wananchi na serikali ya Tanzania juu ya kuwepo ama kutokuwepo kwa njaa nchini, kuna matukio yameanza kujitokeza ambayo yanaashiria kuwepo kwa njaa kwa raia. Miongoni mwa matukio yaliyobainisha kuwepo kwa njaa kwa wananchi ni vitendo vya wanaume wilayani Sengerema hususan katika kijiji cha Isome, kuwatelekeza wake na familia zao kwa ujumla kutokana na kuishiwa uwezo wa kulisha familia zao pamoja na ugumu wa maisha kwa ujumla.
Taarifa hizo zilitolewa na Mwandishi wa habari, Dotto Bulendu kupitia Radio Deutsche Welle, baada ya kutembelea katika wilaya hiyo na kuzungumza na baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo.
Katika mahojiano aliyoyaendesha Dotto Bulendu baina yake na wanachi wanaoishi katika kijiji cha Isome, yalibaini kuwa baadhi ya wanaume wametelekeza familia zao na kukimbilia kusikojulikana hali inayopelekea wake zao kukimbilia au kuhamia kwa wenyeviti wa vijiji au vitongoji kwa ajili ya kuomba misaada ya hifadhi na chakula.
Wakielezea wanawake waliokimbiwa na waume zao, walisema hali ya maisha imekuwa ngumu sana kutokana na baa la njaa, na ukizingatia wana watoto wadogo.
"Siku ya kwanza nilienda kwa jirani nikaomba unga nikawapikia watoto. Siku ya pili nikaenda kwa mwenyekiti. Ameniacha yaani na chakula hamna, mpaka sasa nina mwezi mzima kabisa" Alisema mmoja wa wanawake walioachwa na waume zao ambaye kwa sasa anaishi kwa mwenyekiti wa kijiji hicho.
Aidha, baada ya kuona baa la njaa linazidi kukua huku mvua hazinyeshi wakazi wa kijiji hicho waliamua kuchangishana pesa kwa ajili ya kumlipa mganga wa kienyeji ambaye walitarajia angefanikisha kuleta mvua kijijini hapo, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda kwani mvua hazikuweza kunyesha na hali ya maisha inazidi kuwa ngumu.
"Kwa mawazo ya watu wengine, walipata nafasi ya kuomba mtu wa kutuletea mvua, na wananchi wamechanga shilingi elfu moja, lakini hakuna mafanikio..." Alisema mwananchi mmoja katika mahojiano ya Dotto Bulendu.
Njaa nchini inasababishwa na mvua kutokunyesha kwa muda mrefu kwa maeneo mengi, hali inayopelekea vyakula kupanda bei na kufanya watu kushindwa kumudu bei hiyo, na matokeo yake ni watu kukataa tamaa kama ilivyotokea katika kijiji cha Isome, wilayani Sengerema.
Wengine wanasoma hizi:
Habari za michezo
Timu zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi Zanzibar 2017
Yanga yaichapa 2-0 Zimamoto FC
Simba SC yazidi kusonga mbele kwenye michuano ya Mapinduzi Cup
Simba SC yailambisha mabao 2-1 timu ya Taifa Jang'ombe
Yanga yaichapa Jamhuri mabao 6-0 katika michuano ya Mapinduzi Cup
No comments:
Post a Comment