Wilaya ya Nzega
Tabora, TanzaniaWilaya ya Nzega ni miongoni mwa wilaya saba (7) zinazounda mkoa wa Tabora. Wilaya hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 9226, na inapakana na wilaya ya Igunga kwa upande wa Mashariki, wilaya ya Tabora Mjini (Manispaa) kwa upande wa Kusini na wilaya ya Kahama upande wa kaskazini-magharibi.
Wenyeji wa wilaya ya Nzega ni wanyamwezi. Makabila mengine ambayo yanapatikana katika wilaya hii ni Wasukuma, Waha, Wanyiramba, wachaga, pamoja na waarabu ambao waliingia wilayani humo kwa sababu mbalimbali ikiwemo biashara, ajira na kutafuta maisha kwa ujumla. Wakazi wa wilaya hii wanaishi kijamaa bila kujali makabila au machimbuko yao.
Wilaya hii ina ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo, na inapokea mvua 9,000mm kwa mwaka. Mazao makuu yanayozalishwa katika wilaya hiyo ni pamoja na Mpunga, Mahindi, Mtama, Karanga, Njugu Mawe, Alizeti pamoja na Pamba. Shughuli nyingine inayofanyika hapo wilayani ni ufugaji wa ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku.
Dini kuu katika wilaya hii ni Uislam, Ukristu na asilimia kubwa ya watu waishio maeneo ya vijijini bado wanaamini dini za jadi.
Kwa upande wa kiutawala wilaya ya Nzega ina jumla ya tarafa 4 ambazo ni Bukene, Puke, Nyasa pamoja na Mwakalundi. Pia wilaya hii ina jumla ya kata 46. Halikadhalika ina jumla ya majimbo 3 ya uchaguzi (ubunge), ambayo ni Nzega mjini, Nzega vijijini pamoja na Bukene.
Kwa sasa jimbo la Nzega mjini linashikiliwa na Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe (CCM). Jimbo la vijijini analishikilia Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla (CCM), na jimbo la Bukene linashikiliwa na Mheshimiwa Selemani Zedi (CCM).
Kwa upande wa Mawasiliano, wilaya ya Nzega ni sehemu inapopita barabara inayotoka Dar Es Salaam kuelekea Rwanda na Burundi. Pia kuna barabara inayotoka Tabora mjini kuelekea Mwanza, na yenyewe pia inapita Nzega Mjini na barabara zote hizo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Baadhi ya barabara za mitaa ya Nzega mjini zimewekewa lami na nyingine zimewekewa molamu (changarawe). Pia reli ya kati kutoka Dar Es Salaam kwenda Mwanza, inapita Nzega.
Mawasiliano ya simu za mikononi ni mazuri na matumizi ya simu za mikononi yanazidi kukua katika wilaya ya Nzega kila kukicha, ukilinganisha na miaka kumi iliyopita ambapo ni watu wachache sana ndio walioweza kumiliki simu wilayani humo.
Ongezeko la matumizi ya simu limerahisisha sana mawasiliano, kuanzia kupiga simu za kawaida, kutuma jumbe fupi za maadishi, hadi kutumiana picha na vipande vya video. Siku hizi wakazi wa Nzega wanapashana habari kwa njia ya haraka zaidi kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Facebook, Instagram, Twitter, Imo, n.k.
Wilaya hii haina kituo hata kimoja cha redio wala Televisheni, watu wanapata habari kwa kusikiliza/kutazama radio/TV za nje ya wilaya hali inayopelekea kutokujua shughuli mbalimbali zinazofanyika katika wilaya yao.
Kwa upande wa huduma za kijamii, ni kwamba kwa miaka ya hivi karibuni serikali imejitahidi kujenga shule nyingi za sekondari pamoja na kuongeza shule za msingi ukilinganisha na miaka kadhaa nyuma ambapo shule za sekondari zilikuwa 3 tu katika wilaya nzima ya Nzega.
Serikali inafanya juhudi ya kujenga shule za sekondari zitakazoweza kutoa elimu ya kidato cha nne na cha 6 pamoja na kuzipandishia hadhi shule kadhaa ili ziweze kutoa elimu ya kidato cha 5 na 6 wilayani humo. Wilaya ya Nzega ina chuo kimoja cha ualimu.
Wilaya ya Nzega kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji, lakini kwa siku za hivi karibuni serikali imeweza kuwapa matumaini wananchi wa Nzega ya kuondoa uhaba huo baada ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuridhia ombi la Mbunge wa jimbo la Nzega mjini (CCM), Hussein Mohamed Bashe, la kumuomba Rais asaidie katika mradi wa kuvuta maji ya ziwa victoria.
Kwa sasa wananchi wa Nzega mjini wanapata maji kupitia mradi wa Bwawa la Kage, lililopo uchama, nje kidogo ya mji wa Nzega.
Huduma ya umeme inapatikana maeneo ya mjini Nzega na maeneo mengine yenye mwamko wa biashara hususani yaliyopo pembezoni mwa barabara.
Wilaya ya Nzega ina hospital kubwa 2 ambazo ni ile ya Halmashauri ya wilaya pamoja na ya Ndala ambayo ipo chini ya kanisa. Serikali imejitahidi kujenga Zahanati katika kila kata na kwenye baadhi ya vijiji, lakini pamoja na jitihada hizo, huduma za afya wilayani humo sio nzuri.
Taarifa hii imeandaliwa na mwandishi wetu, kama ina mapungufu au makosa tujulishe
Habari zinazosomwa zaidi
Ziara ya RC Paul Makonda jijini Dar yaibua makubwa
ifahamu kiundani wilaya ya Igunga
Ufahamu mkoa wa Tabora
Zinazofanana na hii
Mkoa wa TaboraWilaya ya Nzega
Wilaya ya Tabora
Wilaya ya Igunga
Wilaya ya Urambo
Maofisa wa mbunge, wataalam wa maji na wenyeviti wa mitaa mjini Nzega wafanya kikao
Mjue Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Mohamed Bashe
Wauza mkaa waua mlinzi wa misitu, Nzega mkoani Tabora
Paul Makonda aanza ziara ya siku 10 ndani ya jiji la Dar Es Salaam
November 19, 2016
Rais Magufuli afanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi za mashirika ya hifadhi za jamii
November 19, 2016
Dr. Shein azindua wodi ya watoto na wazazi
November 19, 2016
Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA
November 20, 2016
No comments:
Post a Comment