Yanga yaichapa tatu bila Timu ya Mafunzo FC
Klabu ya Yanga FC imeyaanza vizuri mashindano ya kombe la Mapinduzi, Zanzibar baada ya kufanikiwa kufunga magoli 3-0 dhidi ya klabu ya Mafunzo FC.
Mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka mwezi januari, yameanza leo katika uwanja wa Amaan mjini Unguja ambapo mechi ya kwanza ilizikutanisha timu za yanga FC na Mafunzo FC.
Kati ya Magoli hayo matatu ya Yanga FC, magoli mawili yalifungwa katika kipindi cha kwanza cha mchezo na mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Dombo Ngoma, na goli la tatu lilifungwa na mshambuliaji mpya, Paul Nonga.
Bao la kwanza liliingia wavuni kunako dakika ya 31 ya kipindi cha kwanza na dakika 2 baadae bao la pili lilifanikiwa kupenya katika lango la Timu ya Mafunzo FC.
Baada ya kuingia uwanjani dakika ya 88 ya mchezo huo, Paul Nonga alifanikiwa kufunga bao la tatu kunako dakika ya 89 alipoachia shuti kali katika lango la timu ya Mafunzo na kupelekea mlinda mlango kulitema.
Katika kipindi cha kwanza Mafunzo FC ilionesha mchezo mzuri ambapo mara kadhaa ilikosa magoli katika lango la timu ya yanga, na katika kipindi cha pili yanga walibadilika na kuutawala mchezo, wakicheza kwa dharau dhidi ya Mafunzo FC.
Kikosi cha Yanga FC kilikuwa na wachezaji wafuatao: Deogratius Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Juma Abdul, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, Simon Msuva/Malimi Busungu dk88, Thabani Kamusoko/Jerome Sina dk70, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk88, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Geofrey Mwashiuya dk70.
Kikosi cha timu ya Mafunzo FC kilikuwa na wachezaji wafuatao: Khalid Mahadhi, Juma Mmanga, Samih Nuhu/Haji Ramadhani dk58, Kheri Salum, Hassan Juma/Haji Abdi dk66, Abdul Hassan, Ali Juma/Jermaine Seif dk72, Sadick Habib/Shaaban Ali dk58, Mohammed Abdul na Ali Mmanga.
Timu za Mafunzo na Yanga FC zimepangwa katika kundi B kwenye ligi hiyo ambayo itatia nanga mnamo tarehe 13 mwezi huu. Timu nyingine zilizopo katika kundi hilo ni pamoja na Azam FC pamoja na Mtibwa Sugar.
Paul Makonda aanza ziara ya siku 10 ndani ya jiji la Dar Es Salaam
November 19, 2016
Rais Magufuli afanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi za mashirika ya hifadhi za jamii
November 19, 2016
Dr. Shein azindua wodi ya watoto na wazazi
November 19, 2016
Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA
November 20, 2016
No comments:
Post a Comment